MIKWARA ya Simba ambayo jana Jumatano jioni ilitua hapa
Shinyanga, imeitia mchecheto Stand United na kupiga chini baadhi ya
vigogo wake pamoja na kuwaweka pembeni kwa muda wengine.
Simba ambayo imerudi kwenye kasi yake katika Ligi
Kuu Bara, itacheza na Stand Jumapili mjini hapa, katika mechi ya awali
jijini Dar es Salaam Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na timu hiyo ngeni
kwenye Ligi Kuu.
Mashabiki wa Simba wameanza kumiminika mjini hapa
huku viongozi wa juu wakionekana hapa na pale kuweka maandalizi sawa
ingawa mashabiki wa Stand ambayo wamechanganyika na wale wa Yanga
wameonekana kujidhatiti vilivyo.
Tayari Stand imewasimamisha kazi viongozi wa
ufundi ambao ni Mkurugenzi wake, Muhibu Kanu, Kocha Msaidizi Emmanuel
Masawe na wachezaji wake watatu Iddi Mobi, Khamisi Shengo na Mussa
Kimbu.
Katibu Msaidizi wa klabu hiyo, Kennedy Nyange alisema uamuzi huo umefanyika wikiendi iliyopita kwenye kikao chao cha ndani.
Barua aliyoandika na Katibu wa Stand United,
Soclaf Mkavilavya ilieleza kuwa Kanu alisimamishwa kwa sababu ameshindwa
kutekeleza majukumu yake na kusababisha usumbufu kwa viongozi.
Pia barua hiyo ilimtaka akabidhi nyaraka zote za
klabu na asiendelee kujishughulisha na shughuli yoyote ya kiutendaji na
atalipwa nusu mshahara kila mwezi hadi hapo uamuzi mwingine
utakapofikiwa, kama hataridhishwa ana haki ya kukata rufaa. Kanu alisema
hatambui kusimamishwa wala tuhuma zake.
Mbali na mechi ya Simba Jumapili, mechi nyingine siku hiyo ni Azam na Tanzania Prisons pamoja na Yanga na Mbeya City.
0 comments:
Post a Comment