MWAMUZI ambaye Yanga wana bifu naye, Martin Saanya amekabidhiwa
kuchezesha mechi ya watani wa jadi Jumapili ijayo, Mwanaspoti
limethibitisha. Mwamuzi huyo mwaka 2009 alikuwa wa akiba wakati Yanga
ilipotoka sare na Simba lakini mwaka 2013 Simba ilipolala mabao 2-0
kwenye Uwanja wa Taifa ndiye aliyechezesha.
Hata hivyo, aliingia kwenye mzozo na Yanga baada
ya kutoa penalti kwa Coastal Union kwenye dakika za lala salama na mechi
kumalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye msimu wa 2012/13, jambo ambalo
liliifanya Yanga kumchukia na kukosa imani naye.
Saanya ambaye alifungiwa na Shirikisho la Soka la
Tanzania (TFF) mwaka mzima kwa kushindwa kumudu mechi hiyo ambayo
ilisababisha mashabiki wa Yanga kuharibu mali za Uwanja wa Mkwakwani
pamoja na basi la Coastal Union.
Kabla ya mchezo huo, mwamuzi huyo alikuwa
akituhumiwa na mashabiki wa Yanga kwamba aliibeba Simba kwenye mechi ya
hisani dhidi ya Azam. Simba ilishinda mabao 3-2 huku Azam wakidai
kunyimwa penalti mbili za wazi.
Habari kutoka ndani ya TFF zimedai kuwa mwamuzi
huyo mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ndiye
atakayeamua nani mbabe katika mechi hiyo ambayo itashuhudia Kocha
Mserbia, Goran Kopunovic akiiongoza Simba kwa mara ya kwanza kwenye
mechi ya watani wa jadi nchini.
Tayari Simba wametimka Jiji la Dar es Salaam na
kwenda visiwani Unguja ambako mara nyingi wanaamini wakitokea huko
hupata matokeo mazuri kutokana na utulivu wa mazingira ambao unawafanya
akili zao zitulie katika jambo moja tu.
Saanya amewahi kuichezesha mechi ya Simba na Yanga
mara moja msimu wa 20012/13 kabla ya kufungiwa na matokeo ya mechi
hiyo ilikuwa ni sare ya bao 1-1. Simba ilianza vibaya ligi hiyo na
ilijikongoja na kupanda mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa
na pointi 23 na itaingia uwanjani ikitoka kuifunga Prisons mabao 5-0
wakati Yanga yenyewe inaongoza ligi ikiwa na pointi 31 na tayari imefuzu
hatua ya pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa
BDF XI ya Botswana na sasa itakutana na Platinum ya nchini Zimbabwe.
0 comments:
Post a Comment