NGASA AIPA MASAA 24 YANGA
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, ametoa saa 24, kumalizia deni analodaiwa shilingi milioni 45 na madai yake ya mishahara ya miezi miwili, ambayo kama hatalipwa, basi ataondoka kambini na kwenda nyumbani kwake.
Timu hiyo imeweka kambi yake Tansoma Hotel, Kariakoo jijini Dar es Salaam, ikijiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF XI FC ya Botswana, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, keshokutwa Jumamosi.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni dakika chache baada ya kuahidiwa kusaidiwa kulipwa deni hilo alilolikopa Benki ya CRDB, fedha zilizotumika kulipia deni la Simba ambalo ni shilingi milioni 35 na fidia ya milioni 10 alizotakiwa kulipa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kusaini timu mbili tofauti.
Ngassa, kama akiondoka kambini, basi hilo litakuwa tukio la pili kwa kiungo huyo kulitenda, aliwahi kuondoka wakati timu hiyo inajiandaa na mechi ya ligi dhidi ya Polisi Morogoro baada ya kudai viongozi wa Yanga kumsusia deni lake hilo.
Akizungumza na Championi Jumatano muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano na waandishi wa habari, Ngassa alisema kiukweli kabisa hadi kufikia siku ya Alhamisi yaani kesho kama hawajalipiwwa hilo deni, mashabiki wa Yanga watamsamehe na ataondoka kambini hapo na hatacheza mechi ijayo.
Ngassa alisema anawaheshimu na anawapenda mashabiki wa Yanga lakini umefika wakati wa kuangalia maisha na siyo kucheza soka kwa sifa zaidi.Alisema ataondoka kambini kwa ajili ya kwenda kutafuta fedha za kumuuguza mke wake aliyefunga naye ndoa hivi karibuni ambaye ni mgonjwa.
“Nikwambie ukweli tu, awali nilipanga kutoingia kabisa kambini, lakini baada ya kukaa na viongozi na kukubaliana, nimeona niingie kambini kwa makubaliano kuwa hadi kufikia keshokutwa (Alhamisi) (yaani saa 24 toka leo), hela yote iwe imeingizwa benki.
“Na kama hawataingiza hizo fedha benki, basi nitakubali yaishe, nitawaaga mashabiki wa Yanga na kuondoka kambini, ninawapenda sana na nawashukuru kwa sapoti kubwa wanayonipa kipindi chote nikiwa Yanga.
“Ninawapenda mashabiki wa Yanga lakini katika hili sitaweza kuvumilia, nitaondoka zangu, nilikubali kukatwa deni kubwa nililolikopa benki kwa makubaliano ya kunisaidia kulipa, nilikubali tena kukaa Yanga bila ya kulipwa mishahara yangu ya miezi miwili, wa Oktoba na Januari, lakini sasa nimeshindwa.
“Hivyo sioni sababu ya kuendelea kukaa kambini huku mke wangu akiwa mgonjwa akihitaji matibabu huku nikiwa sina fedha za kumuuguza,” alisema Ngassa.
0 comments:
Post a Comment