Dodoma/Dar. Wakati wowote wiki hii, Rais Jakaya Kikwete
anatarajia kukutana na viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete atakutaka
‘kiaina’ na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao
unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa Ukawa na baadhi
kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM
kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa
katika Rasimu.
TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi
bungeni ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, huku
vyama visivyo na uwakilishi bungeni vikiwakilishwa na UPDP
kinachoongozwa na Fahmi Dovutwa.
Jana, kwa nyakati tofauti wenyeviti wenza wa
Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James
Mbatia (NCCR Mageuzi), walisema wako tayari kukutana na Rais, ila
msimamo wao wa kutaka ijadiliwe rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Ukawa kuomba
wakutane na Rais Kikwete kwa ajili ya kujadiliana namna bora ya
kuendesha mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma
jana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema Rais atafanya kikao hicho
wakati wowote ndani ya wiki hii na kwamba viongozi wa vyama wakiwamo wa
Ukawa, wamethibitisha kushiriki.
Cheyo alisema, katika kikao walichokutana Dar es
Salaam Agosti 23, wanachama wa TCD walikubaliana kwamba upo umuhimu wa
kukutana na Rais Kikwete kwa mazungumzo na maridhiano.
Kukutana kwa viongozi hao, kunakuja huku wajumbe
wa Bunge Maalumu wakiwa wamemaliza kujadili sura zote 15 zilizokuwa
zimesalia na tayari baadhi ya kamati zimemaliza kupiga kura wakisubiri
kuingia bungeni Septemba 2 kwa kazi ya kupigia kura sura kwa sura.
Kuhusu viongozi wa Ukawa, alisema wanazo taarifa
na baadhi yao walikuwapo katika kikao cha kujadili kukutana na kiongozi
huyo wa nchi, hivyo akasema lazima watashiriki wakati wowote wakiitwa.
Lipumba
Akizungumzia mkutano huo na Rais, Profesa Lipumba
alisema: “Tunakutana na Rais Kikwete kwa sababu sisi ni wanachama wa
TCD.” Alipoulizwa juu ya msimamo wa Ukawa, alisema lengo ni kutafuta
mwafaka ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uendeshwe kwa kufuata sheria,
kanuni na taratibu.
0 comments:
Post a Comment