Arusha. Mchakato wa kuandika Katiba Mpya
unaoendelea mjini Dodoma umekumbwa na mizozo hasa baada ya wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kususa na kutorejea Dodoma.
Wajumbe hao wamekuwa wakitaka kwanza, kuheshimiwa
maoni ya wananchi yaliyowasilishwa bungeni humo kupitia rasimu ya pili
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba .
Ukawa, pia wamekuwa wakipinga lugha za kejeli,
matusi katika Bunge hilo, sambamba na kupitishwa kwa kanuni mpya wakati
wakiwa nje ya bunge hilo, kanuni ambazo wanaeleza zitaathiri rasimu ya
tume iliyopo bungeni.
Vikao kadhaa vya maridhiano vimekuwa vikiendelea
kukwama na hivyo upande mmoja, yaani CCM umeamua kuendelea na vikao vya
bunge hilo.
Kutokana na hali hiyo, maoni mbalimbali yamekuwa yakitolewa ili kunusuru mchakato huo ambao ni dhahiri umekwama.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dk
Raphael Chegeni katika mahojiano na gazeti hili anashauri Bunge
lisitishwe ili kuepuka kutumia vibaya fedha za umma.
Swali: Dk Chegeni wewe ni kada wa CCM kwa nini sasa unashauri bunge kusitishwa kwa sasa?
Jibu: Mimi naamini baada ya wajumbe wa kundi la
Ukawa kususia bunge hilo hakutawezekana kupatikana kwa kura ya uamuzi ya
theluthi mbili kuwezesha kupatikana kwa Katiba mpya.
Kwa mujibu wa kifungu cha 26(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili Katiba
Mpya inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu la Katiba itahitaji kuungwa
mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote kutoka
Tanzania Bara, na theluthi mbili ya wajumbe wote
kutoka Zanzibar. Kwa hali hii, si rahisi kwa upande wowote kupata
theluthi mbili.
0 comments:
Post a Comment