Washitakiwa
Patrick Natala na Maxmillian Msacky (katikati) wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar kutengeneza tovuti bandia.
WATU wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wakituhumiwa kughushi, kutengeneza tovuti bandia na mifumo ya
mtandao kwa kutumia majina ya baadhi ya viongozi wa Serikali, likiwemo
la Rais Jakaya Kikwete na taasisi kubwa hapa nchini.Washitakiwa hao ni Patrick Natala na Maxmillian Msacky waliofikishwa mahakamani hapo jana ambapo Mawakili wa Serikali, Theophil Mutakyawa akisaidiwa na Wakili Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungura, waliwasomea washitakiwa hao mashitaka 10.
Washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Januari na Aprili, 2014, walitengeneza tovuti bandia kwa kutumia majina ya Taasisi ya Jakaya Kikwete Foundation (Ikulu), TCRA Foundation, Akiba Saccos Social Company, Social Credit and Loans Company, Ridhiwani Social Company, Hisa Tanzania, Zitto Kabwe Foundation, Vicoba Tanzania na Wekeza Fund.
Aidha, Msacky anadaiwa kati ya mwaka 2006 na 2014 kwa njia ya udanganyifu alighushi cheti cha sekondari namba 0421130 chenye namba S 0260-0001 na kati ya 2005 na 2014 alighushi cheti cha sekondari namba 0217951 chenye namba S 0310-0532, akionesha ni halali na vimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania, jambo ambalo si kweli.
Mutakyawa aliendelea kudai kuwa, kati ya 2006 na 2014, Msacky alighushi cheti chenye namba 2004-120202 kwa madai ni halali kimetolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Kompyuta jambo ambalo si kweli.
Aidha, ilidaiwa kati ya 2010 na 2014 alighushi cheti cha matokeo chenye usajili namba 7703/T.07 akidai ni halali na kimetolewa na Chuo Kikuu cha Mzumbe, jambo ambalo si kweli.
Aliendelea kudai kuwa, kati ya 2010 na 2014 anadaiwa kughushi cheti cha elimu ya juu namba 6109 akidai ni halali na alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe baada ya kupata Shahada ya Sayansi ya Teknolojia ya Mawasiliano na Utawala.
Anadaiwa Julai 2014 aliziwasilisha nyaraka hizo za kughushi katika ofisi ya SB Enterprises iliyopo Barabara ya Nyerere kwa lengo la kutafuta ajira. Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, washitakiwa wamerudishwa rumande hadi Septemba 28, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment