Shirikisho la soka nchini Tanzania
(TFF) litatoa ujumbe maalumu siku ya Jumapili wakati wa mechi ya watani
wa jadi , Simba na Yanga kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
(albino).Mauji ya albino yamekuwa yakijirudia nchi Tanzania kwa imani
potofu za kishirikina kwa imani kuwa sehemu ya viungo vyao vya mwili
vinasababisha mtu kupata utajiri.
Kuelekea mechi ya ligi kuu nchini Tanzania kati ya watani wa jadi , homa imepamba moto na kwa hesabu za haraka haraka, mashabiki wapatao milioni 10 watakosa raha, ama kupata furaha kwa dakika 90 siku ya Jumapili wakati Simba na Yanga zitamenyana katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tayari majigambo yameanza na timu hizo mbili, moja ya timu kongwe barani Africa zikiwa na zaidi ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, zimeanza kambi maalumu kujiandaa na mechi hiyo muhimu, ambayo wakati mwengine hupelekea hata makocha kufukuzwa kazi, kwani ni kama mtaji wa uongozi.
Tayari, kocha wa sasa wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic ametabiri mechi ya kukata na shoka, akiwaelezea Yanga kama kikosi kilicho vizuri msimu huu katika kugombania ubingwa na kwa sasa ikiongoza ligi ikiwa na pointi 31.
Kopunovic amesema anategemea kupata ushindi dhidi ya Yanga licha ya kuwa nafasi ya 5 katika msimamo (ikiwa na pointi 23), baada ya kusuasua kupata ushindi katika mechi kadhaa zilizopita na zile za mwanzo wa msimu wa ligi, ikiwa na rekodi ya kupata droo mfululizo katika mechi saba, ikiwa chini ya kocha aliyetupiwa virago, Mzambia Patrick Phiri.
Mhasimu wake, kocha Mdachi wa Yanga, Hans Pluijm, akilindwa na rekodi ya ushindi mfululizo katika mechi za ligi kuu na zile za michuano ya kombe la Vilabu barani Afrika, amesema kocha yeyote ana mategemeo ya ushindi, hivyo vijana wake, wana ari ya kushinda.
Mechi ya Simba na Yanga huvuta hisia za watu wengi nchini Tanzania nakusababisha baadhi ya mashabiki kuzimia uwanjani kutokana na presha, ama ya ushindi au kufungwa. Licha ya ligi kuu kuwa na timu 14, timu hizo mbili ndizo zinazoongoza kuwa ma mashabiki wengi zaidi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.
chanzo:BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment