Ndugu wa marehemu walifichua siri hiyo wakati wakizungumza na
NIPASHE kwenye mazishi ya kijana huyo yaliyofanyika jana eneo la
Malamba Mawili Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam.
Kaka wa marehemu, Abdallah Yusuf, alisema Farahani (marehemu),
kabla ya mauti hayo kumkuta, alikuwa akitoa fedha kwa awamu kwa ajili ya
kununulia gari la kusombea mchanga ‘tiper’ kwa bei ya Sh. milioni 35.
Alisema katika makubaliano hayo, Farahani alianza kutoa Sh. milioni
17, mara ya pili milioni 10, mara ya tatu Sh. 500,000 na baadaye
akamalizia kwa kutoa Sh. 2,500,000 ambazo alimkabidhi rafiki yake na
mtuhumiwa siku moja kabla ya mauti kumkuta.
Alisema mdogo wake alipotea Juni 11, mwaka jana na taarifa zilitolewa katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuf.
Abdallah alisema baada ya uchunguzi kufanyika, polisi walifanikiwa
kumkamata mtuhumiwa ambaye ni Hemed Hamis na kumuweka kituoni kwa muda
wa wiki mbili kabla ya kutolewa nje kwa dhamana kwa madai alikuwa
mgonjwa.
“Mdogo wangu alivyopotea nilikuwa natumiwa meseji kupitia simu yake
ambazo zilikuwa zinasema `mdogo wako huwezi kumpata hadi pale
utakapokuja kunikabidhi fedha zangu Shilingi milioni 75 ,” alisema.
Alisema simu hiyo iliendelea kutumiwa kwa mwezi mmoja na baada ya
hapo haikupatikana tena, kitendo kilichowafanya ndugu kukutana kujadili
suala hilo na baadaye walikata tamaa.
“Tulikata tamaa kumtafuta baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila
mafanikio na pia simu tulizokuwa tunapigiwa zilikuwa hazipatikani tena,”
alisema na kuongeza:
“Pia simu za vitisho zilitupa wasiwasi na kudhani mdogo wetu
alishiriki vitendo viovu ambavyo vilitufanya tuamini kuwa mdogo wetu
ametoroka kwenda nje.”
Naye dada wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini,
alisema Jumatatu wiki hii, walipigiwa simu na polisi wa Kituo cha
Polisi Mbezi kwa Yusuf na kuwataka waende Kituo cha Polisi Msimbazi.
Alisema baadaye kaka yao ambaye ni Abdallah, aliporudi kutoka Kituo
cha Polisi Msimbazi, aliwaeleza kuwa Faharani (marehemu), aliuawa na
rafiki yake Hemed na alimfukia kwenye nyumba aliyokuwa anaishi.
Aliongeza kuwa polisi waliwachukua ndugu zao wa kiume na kwenda nao
katika nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa (Hemed) iliyopo eneo la Ilala
Sharif Shamba, jijini Dar es Salaam.
Alisema walipofika katika nyumba hiyo, walionyeshwa eneo ambako
Farahani alikuwa amezikwa na kuanza kuufukua mwili wake na kuuchukua
kwenda nao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya
uchunguzi.
Hata hivyo, zoezi la kufukua mwili huo lilikuwa na changamoto
kutokana na mtuhumiwa kuonyesha eneo la uani ambalo halikuwa lenyewe.
Jirani mmoja ambaye alikuwapo eneo la tukio, aliwaonyesha polisi
eneo ambalo alikuwa na shaka nalo na ndipo polisi walipoanza kufukua
mwili huo.
Taarifa zinaeleza kuwa kazi ya kufukua mwili wa marehemu huo
ulianza saa 4:00 asuhubi na kumalizika saa 8:00 kutokana na shimo
alilokuwa amezikwa kuwa na urefu wa mita 10.
Naye Mustapha Mwalongo, aliyekuwa akifanya kazi na marehemu,
alisema alimfahamu Farahani kuwa mfanyakazi wa mabasi ya kampuni ya
Noraz na Waheed.
Alisema alimuamini Hemed kwani alikuwa ni mtoto wa bosi wake na aliyekuwa karibu naye.
Mwalongo ambaye pia ni Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi
Tanzania (Taboa), alisema kufuatia marehemu kumdai sana mtuhumiwa,
ilifikia hatua akamweleza baba yake na mtuhumiwa, hali iliyosababisha
urafiki wao kuvunjika.
Kwa upande wake, rafiki wa karibu wa marehemu, Somji Nawanda,
alisema Hemed (mtuhumiwa), alimpigia simu marehemu Juni 9, mwaka jana na
kumtaka aende Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kulipia
ushuru wa gari alilomwagiza.
Alisema alipofika TRA, walimtafuta Hemed ambaye alidai kuwa muda
huo alikuwa Kariakoo na baadaye alimpigia simu na kumwambia aonane na
mtu mmoja aitwaye Said amkabidhi Sh. milioni 2.5.
“Marehemu alisita, lakini Hemed alimwambia ni pesa ngapi umenipa
unashindwa kuniamini kwa fedha hizo? Ndipo marehemu alipomkabidhi fedha
hizo Said na kumwambia asubiri aingie TRA amchukulie stakabadhi,
aliporudi Said alisema mtandao unasumbua hivyo hawezi kupata stakabadhi
waonane naye tena Juni 11, mwaka jana kwa ajili ya kuchukua gari,”
alisema Nawanda.
Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kuwa ni Mama Salum, alisema
hawakuwa na taarifa kama jirani yao alifariki dunia kutokana na kazi
zake za uwakala ila walidhani amesafiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alipotafutwa juzi kwa
njia ya simu, alisema alikuwa barabarani akiendesha gari na kuahidi kuwa
akishuka atapiga simu.
Hata hivyo, baada ya kuendelea kupigiwa simu, alituma ujumbe mfupi (sms) akisema kuwa angepiga muda mfupi, ingawa hakupiga.
Hata alipopigiwa na kutumiwa sms, hakupokea hadi tunakwenda mitamboni.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
alipopigiwa awali, alielekeza apigiwe Nzuki, akisema kuwa ndiye mwenye
taarifa hizo.
Jumatatu wiki hii, polisi, ndugu na wakazi wa Ilala Sharif Shamba,
jijini Dar es Salaam, walifichua kuuawa kwa Farahani aliyeuawa na rafiki
yake kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulifukia pamoja na
kulisakafia uani kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.
0 comments:
Post a Comment