PHIRI APEWA MECHI TANO SIMBA

Kocha mkuu wa Simba, Mzambia, Patrick Phiri.

ALIYEWAHI kuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’, ameibuka na kuwataka wanachama na mashabiki kutokata tamaa kuhusu mwenendo wa kikosi chao, huku akitoa mechi tano ndipo waanze kujadili ubora wa kikosi chao.
Simba imeanza ligi kwa kusuasua huku ikiwa haijashinda mechi yoyote, zaidi ya kuambulia sare katika michezo yote miwili, licha ya ‘kuangamiza’ mamilioni kuwasajili nyota ndani na nje ya nchi.
Hali hiyo imewafanya baadhi ya wanachama kuanza kukikatia tamaa kiwango cha timu yao chini ya kocha mwenye rekodi ya heshima klabuni hapo, Mzambia, Patrick Phiri.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mzee Kinesi ambaye ameamua kupumzika baada ya kumaliza muda wake katika uongozi uliopita chini ya Ismail Aden Rage, alizitaja sababu zinazoifanya Simba kuboronga mpaka sasa kuwa ni mabadiliko ya uongozi.
“Kwangu sioni kama Simba ina mwendo mbaya. Labda hali iliyopo imetokana na mabadiliko kwenye ngazi ya uongozi pamoja na kuwepo kwa wachezaji wengi wapya.
“Hivyo, wachezaji hawajazoeana kuweza kucheza kitimu, nafikiri viongozi wa juu wanafuatilia mwenendo na wanampima kocha labda baadaye wanaweza kusema chochote,” alisema Kinesi na kuongeza:
“Phiri naye ni binadamu, hakuna aliyekamilika. Anaweza kuwa katika ubora wake au akashuka kiuwezo, lakini ni mapema sana kumjadili, labda baada ya mechi tano au sita ndipo anaweza kufanyiwa tathmini katika mwenendo wa timu nzima.”
Simba ipo nafasi ya kumi ikiwa na pointi mbili, baada ya kulazimishwa sare na timu za Coastal Union na Polisi Morogoro huku ikijiandaa kuwakaribisha Stand United wikiendi hii.
Share on Google Plus

About ahmed

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment