WANAWAKE: MSITUMIE SUKARI SIYO NZURI SANA!

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na jarida moja la masuala ya afya la nchini Uingereza (BMC Public Health), unywaji wa vinywaji vyenye sukari, kiasi cha mara tatu kwa wiki, huweza kunenepesha matiti na unenepaji wa matiti huongeza hatari ya mwanamke kupatwa na saratani ya matiti.
Waliofanyiwa utafiti huo ni wanawake 776 ambao hawajafikia ukomo wa hedhi (Premenopausal) na wanawake 779 waliofikia ukomo wa hedhi (Postmenopausal).
Pamoja na maswali mengine waliyoulizwa, wanawake hao waliulizwa kiasi wanachokula kwa upande wa vyakula na vinywaji vyenye sukari kama vile chokoleti, keki, ice cream, soda, n.k na huwa wanaweka vijiko vingapi vya sukari kwa vinywaji wanavyotayarisha, kama chai au juisi.
Akiongelea matokeo ya utafiti wao, mtafiti na mwandishi kiongozi wa utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Laval cha Quebec, nchini Canada, Caroline Diorio alisema kuwa matokeo yalionesha kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya utumiaji wa sukari kwa wingi na kuongezeka kwa ukubwa wa matiti ya wanawake kutoka makundi yote mawili (wasichana na watu wazima).
Katika utafiti wao, wamegundua zaidi kuwa wanawake waliofikisha ukomo wa hedhi matiti yao yaliongezeka ukubwa zaidi kwa kula vyakula vingi vyenye mafuta, wakati wanawake ambao hawajafikisha ukomo wa hedhi, waliongezeka ukubwa wa matiti yao kwa kula vinywaji vyenye sukari visivyopungua vitatu kwa wiki.
Matokeo ya utafiti huo yanatoa picha kwamba kuwa na matiti makubwa kunakosababishwa na ulaji wa sukari pamoja na mafuta kwa wingi huongeza hatari ya kupatwa na saratani ya matiti kwa asilimia 3.
Dk. Dioro anamalizia kwa kusema kuwa utafiti zaidi unahitajika, hususan katika makundi ya watu wenye matumizi makubwa ya sukari. Lakini hata hivyo, amesema kuwa hadi utafiti mwingine utakapofanyika na kuthibitisha vinginevyo, kwa sasa uhusiano wa matumizi makubwa ya sukari na unenepaji wa matiti kwa wanawake uko wazi.
Kwa kuwa unenepaji wa matiti una uhusiano mkubwa na ulaji mkubwa wa mafuta na sukari kwa njia mbalimbali kama zilivyoanishwa hapo juu, na kwa kuwa unenepaji wa matiti unaongeza pia hatari ya mwanamke kupatwa na saratani ya matiti, ni sababu tosha kabisa ya wewe kuamua kuachana na unywaji wa vinywaji baridi vyenye sukari nyingi kwa faida ya afya yako.
Kama ambavyo mara kwa mara tumekuwa tukisisitiza, tuepuke sana matumizi makubwa ya sukari na tunapoitumia basi tuitumie kwa kiasi kidogo sana na badala yake tupendelee kutumia asali na kula kwa wingi matunda na mboga za majani ambazo huwa na sukari asilia ambayo haina madhara mwilini.
Share on Google Plus

About ahmed

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment