UHAKIKA WA MTAJI
Bila shaka msomaji wangu unaendelea vyema na shughuli zako za ujasiriamali. Mada ya njia za uhakika za kupata mtaji wa kuanzisha biashara ni ndefu lakini naamini kila siku unajifunza kitu kipya chenye manufaa makubwa kwako.
Leo nataka kujadili nawe njia mpya ya kupata mtaji wa kuanzisha biashara ambayo naamini hata wewe unayelalamika kila siku kwamba huna mtaji, inaweza kukusaidia kujikwamua kutoka hapo ulipo.
TUMIA PESA YA MTEJA KUANZISHA BIASHARA YAKO
Unaweza kupata mtaji kwa kufikiri kwa utofauti na watu wengine. Katika njia hii ambayo kijasiriamali huitwa Customer Financing, mteja hukupatia pesa kwa ajili ya wewe kutengeneza bidhaa au huduma anayoihitaji. Kinachohitajika hapa ni uaminifu wa hali ya juu.
Kuna biashara nyingi ambazo huu ndiyo huwa utaratibu wa uendeshwaji wa biashara ambapo mteja hutakiwa kulipa kwanza ndiyo bidhaa au huduma iandaliwe. Mfano, kama una kipaji cha kupika vizuri, unaweza kuanzisha biashara ya ‘catering’ au biashara ya kulisha watu kwenye matukio ya kijamii.
Unachotakiwa kuwa nacho ni kujiamini, kutafuta watu wenye uhitaji na kuwaambia kuhusu biashara yako.
Mteja akikubali atakulipa kabisa na utakachotakiwa kukifanya ni kukodisha vyombo, kukodi wapishi na kununua vyakula kwa ajili ya maandalizi ya shughuli husika kama mchele, nyama, mafuta nk. Baada ya hapo itatakiwa utafute wahudumu wa kukusaidia kugawa chakula na kuwahudumia wahusika wa shughuli yenyewe.
Jambo la kuelewa hapa ni kwamba mjasiriamali ni mtu anayechanganya malighali na watu na kutengeneza tija (value) mahali ambapo kusingekuwa na tija. Kuwa mjasiriamali ni sawa na kuwa mtengeneza filamu ambaye anatafuta wasanii, eneo la kuchukulia filamu, pamoja na vitendea kazi vyote.
Baadaye filamu ikiwa tayari sisi hununua kuangalia na kufurahia wakati yeye akiwa ameshaingiza pesa yake.
Mtaji mkubwa hapa huwa ni uamanifu. Hapa kwetu kuna watu wengi wanakwama kila siku kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa wateja wao. Kwa mfano wapo baadhi ya wajasiriamali wanaoendesha biashara ya utalii ambapo kimsingi mteja ambaye yuko Ulaya, Australia, Marekani au Asia hutakiwa kulipia huduma hiyo kabla hajaja nchini.
Kwa sababu ya tamaa, wajasiriamali wengi kwenye fani huishia kutumia pesa hiyo kwa matumizi binafsi na kukosa uaminifu. Mtalii anapofika nchini hupigwa na butwaa kwa kuona kwamba huduma anayopewa ni ya chini sana tofauti na malipo na makubaliano ya awali.
Pia ipo mifano kadhaa ya aibu sana kwa taifa letu ambapo mjasirimali wa soko hili akishalipwa hutokomea kabisa na kumwacha mtalii kwenye mataa. Mara nyingi baada ya kutua uwanja wa ndege na kujaribu kufanya mawasiliano na mhusika, ndiyo anapogundua kwamba mjasiriamali ni tapeli.
Matokeo yake wajasiriamali wachache kama hawa huliabisha taifa letu na kuwaumiza wajasiriamali wengine wa soko la utalii kwa wageni kutilia mashaka huduma zetu kwa jumla. Hivyo kama utapata mtaji kwa njia hii hakikisha unakuwa ni mwaminifu na utabarikiwa na kufika mbali maishani.
Kama unataabika na kukosa uaminifu na tamaa huwa inataka kukuharibia bahati yako kwenye biashara nakushauri upate ushauri wa kitalaamu au wa kiroho mfano kuwaomba watumishi wa Mungu wakuombee, kwani kama hili ni tatizo kwako, hata ungeenda juu kiasi gani,utaanguka siku moja kwa kuwa msingi wako kijasiriamali siyo imara.
Kingine ni kutafuta na kusoma kitabu kinachoitwa The Speed of Trust cha Stephen M.R Covey ambacho ni moja kati ya vitabu bora kabisa ulimwenguni juu ya somo na faida nyingi za uaminifu maishani.
Sehemu nyingine ya wazi ambapo unaweza kutumia pesa ya mteja ni kwenye biashara za mtandao au Multilevel Marketing au kwa kifupi (MLM). Makampuni ya mfumo huu ambayo mengi hutokea Marekani, Asia au Ulaya huwapatia wanachama wake sample za bidhaa zao kwa ajili ya kuwaonesha au kuwaonjesha wateja wapya.
Kama mteja atavutiwa na bidhaa basi hutakiwa kukupatia pesa ili uweze kumnunulia bidhaa kutoka kwenye kampuni husika na kumpelekea pale alipo. Wewe kama mwanachama utaweza kujipatia cha juu (faida) kwani utanunua bidhaa zile kwa bei ya punguzo (membership price) na kumuuzia mteja wako kwa bei ya juu ambayo mara nyingi hupangwa na kampuni.
Watu wengi hapa kwetu wamejikwamua kwa njia hii na kuweza kupata mitaji ya kuendeshea biashara zao binafsi na wengine wengi wameweza kupunguza makali ya maisha kwa njia hii. Pia wapo wachache ambao wamekuwa mamilionea kwa kupitia biashara hizi kwa kufanya kazi kwa bidii sana na kwa muda mrefu bila kukata tamaa.
Wengi wa mamilionea hawa hawakuwa na mtaji wowote walipoanza miaka michache iliyopita zaidi tu ya kuwa na ujasiri wa kuongea na watu wengi kadiri walivyoweza na kuwaomba wateja walipie kwanza bidhaa wanazozihitaji na kuzipokea baadae.
Kama wewe ni mtu unayependa kujichanganya na watu wengine (social), unaweza kujituma na kujisimamia mwenyewe (self motivation) huogopi kukataliwa (rejection) na hukati tamaa kirahisi, basi biashara hii inaweza kukufaa zaidi.
0 comments:
Post a Comment