Ujenzi wa Reli ya kisasa kwa ajili ya Treni za umeme DSM-Morogoro Yazinduliwa Rasmi

Rais John Magufuli aliweka jiwe la msingi la uzinduzi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo katika eneo la Pugu Stesheni wilayani Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.
Awamu hiyo inatarajiwa kukamilika Oktoba 2019, ikianzia Dar es Salaam hadi Morogoro ilizindua safari ya kuelekea katika kuwa na reli ya kisasa (standard gauge) itakayoanzia jijini Dar es Salaam hadi Mwanza, ambayo itakuwa na manufaa makubwa kiuchumi na kijamii na hivyo kulifanya Taifa kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Rais John Magufuli aliweka jiwe la msingi la uzinduzi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo katika eneo la Pugu Stesheni wilayani Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.
Awamu hiyo inatarajiwa kukamilika Oktoba 2019, ikianzia Dar es Salaam hadi Morogoro.
Ujenzi wa reli hiyo, utakaogharimu kiasi cha Sh trilioni 2.7, utaiwezesha Tanzania kwa mara ya kwanza tangu miaka 112 iliyopita ilipojengwa reli ya kiwango cha mita gauge, kuwa na treni ya masafa marefu ya mwendo kasi inayosafiri kwa kilometa 160 kwa saa.

Pamoja na hayo, kukamilika kwa reli hiyo kutaiwezesha Tanzania kuondokana na tatizo la uharibifu wa barabara zake kutokana na mizigo mizito inayosafirishwa na malori, ambapo reli hiyo pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kubeba mizigo hiyo kwa wingi, lakini itaifikisha kwa haraka kwa wamiliki wake.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk Magufuli alisema awamu hiyo ya kwanza itakayokuwa na stesheni sita ikiwemo stesheni kubwa itakayojengwa eneo la Ruvu pamoja na bandari kavu, itakuwa ni kilometa 300.
Alieleza kuwa treni hiyo injini zake zitatumia umeme na mafuta aina ya dizeli, na itakuwa na uwezo wa kwenda Morogoro kutoka Dar es Salaam kwa muda wa saa 1.45.
“Na ikikamilika yote hadi Mwanza, itatumia muda wa saa 2.45 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza itatumia muda wa saa 7.30,” alifafanua.
Alisema tangu mwaka 1899 ilipoanza kujengwa reli ya kiwango cha mita gauge na Wajerumani iliyokamilishwa mwaka 1929 na Waingereza, Watanzania wamekuwa wakitumia huduma za treni hiyo ambayo uwezo wake ni kasi ya kilometa 50 kwa saa.
Hata hivyo, alisema kutokana na uchakavu wa miundombinu ya reli hiyo kwa sasa ina uwezo wa kwenda kilometa 20 kwa saa huku uwezo wake wa kubeba mizigo ukiwa ni tani 500.
Tofauti na treni hiyo, treni ya kisasa ya mwendokasi wa umeme itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 10,000.
Dk Magufuli alisema reli hiyo ya kisasa itakayokuwa na urefu wa kilometa 1,219 na itajengwa kwa awamu tano ambazo ni Dar es Salaam - Morogoro, Morogoro – Makutupora, Makutupora – Tabora, Tabora – Isaka na Isaka – Mwanza.
Alisema kukamilika kwa ujenzi huo, kutaondoa tatizo la usafiri kwa Watanzania na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wa nchi sita zinazopakana na Tanzania, lakini pia kupunguza uharibifu wa barabara unaoendelea kwa sasa kutokana na mizigo mingi kusafirishwa kwa malori.
Alitaja nchi zitakazounganishwa na reli hiyo na kuamsha hamasa ya kibiashara kuwa ni Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini na Burundi.

“Ikikamilika reli hii Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kukamilisha mradi kama huu kwa fedha zake yenyewe, lakini pia itakuwa ni nchi ya pili Afrika baada ya Morocco na Afrika Kusini kwa kuwa na treni ya kisasa inayotumia umeme lakini yenye masafa marefu,” alisema Dk Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema treni hiyo ndio itakayokuwa mkombozi wa barabara ambazo hadi sasa serikali imejitahidi kujenga mtandao wa barabara za lami wa kilometa 17,000 ambazo hata hivyo hazidumu kutokana na kuharibiwa vibaya na mizigo mizito inayosafirishwa na malori.
“Utafiti unaonesha kuwa treni ndio usafiri sahihi wa kusafirisha mizigo. Sasa reli hii tumejipanga ndio iwe mkombozi wa barabara zetu na kuokoa fedha za serikali na kodi za wananchi zinazotumika kila mara kukarabati barabara,” alieleza.
Alisema pia reli hiyo itapunguza tatizo la ajira, ambapo katika shughuli zake za ujenzi inatarajiwa kutoa ajira 600,000 kwa watanzania na kati ya ajira hizo ajira 30,000 zitakuwa ni ajira za moja kwa moja na za kudumu na ajira milioni moja zitatokana na sekta nyingine zinazotumia reli hiyo kama vile viwanda, madini, uvuvi na biashara.
“…Moja ya vikwazo vikubwa cha biashara katika nchi nyingi za Afrika ni ukosefu au ubovu wa miundombinu ya usafiri. Tatizo hili linachangia kuwepo kwa hasara kwenye biashara kwa asilimia 40. Ndio maana miongoni mwa nchi za Afrika biashara iko chini ya asilimia 15, wakati mabara mengine inaanzia asilimia 60 kwenda juu,” alisema.
Alisema serikali hiyo imejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi huku akitolea mfano wa miradi inayoendelea na iliyopo mbioni kuanza, ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Morogoro mpaka Makutupora, ambao tayari Rais wa Uturuki ametuma benki tano za nchi hiyo kufanya mazungumzo na serikali na kuangalia namna ya kuutekeleza.
Miradi mingine ni ujenzi wa daraja katika makutano ya Ubungo, ujenzi wa barabara za juu eneo la Tazara, Aga Khan na Coco Beach ambapo pia Benki ya Dunia imeahidi kutoa dola za Marekani bilioni 300 kwa ajili ya kukarabati reli ya sasa ya kiwango cha mita gauge ili iendelee kutumika.
Alisema pia serikali imeshapata mkopo wa dola za Marekani bilioni 427 kwa ajili ya kuanza kujenga awamu ya pili ya mradi wa mabasi ya mwendokasi, ambapo safari hii ujenzi wake utaanzia eneo la Gongo la Mboto na barabara yake itakuwa ni ya urefu wa kilometa 23.8.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment