LEO Taifa Stars Maboresho inacheza mechi ya
kirafiki na Rwanda ya Haruna Niyonzima kwenye Uwanja wa CCM Kirumba,
Mwanza, lakini Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limefanyia marekebisho
kanuni zake za michuano ya ngazi ya klabu kwa upande wa malazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), CAF imesema kuanzia sasa timu
zitachagua na kujilipia zenyewe hoteli zinapokuwa kwenye mechi za
ugenini.
Kabla ya marekebisho ya kanuni
hiyo, timu ngeni ilikuwa ikilipiwa hoteli na timu mwenyeji kwa msafara
usiozidi watu 25. CAF ilikuwa imepitisha hoteli maalumu katika kila nchi
ambapo mwenyeji alitakiwa kuziweka timu ngeni.
Kwa marekebisho hayo, chama cha
soka cha nchi mwenyeji kitakuwa na wajibu wa kuitafutia hoteli timu
ngeni iwapo tu kitaombwa kufanya hivyo, lakini jukumu la kulipia malazi
litakuwa la timu yenyewe.
Mwaka huu Tanzania inawakilishwa
na timu mbili za Azam na Yanga katika michuano ya CAF ambapo Azam
itacheza Ligi ya Mabingwa na Yanga itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga itacheza Februari 14, mwaka huu na BDF IX ya Botswana na Azam
itacheza na El Merreikh ya Sudan Februari 15 kwenye Uwanja wa Azam
Complex jijini Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Taifa Stars
Maboresho inayoongozwa na Simon Msuva leo Alhamisi inacheza mechi ya
kirafiki na Rwanda ‘Amavubi’ jijini Mwanza kwa lengo kuboresha kikosi
hicho kwani mchezo huo hautambuliwi na Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa).
0 comments:
Post a Comment