Ndugu zangu, hakuna anayeweza kuupinga ukweli kwamba, maisha
ya sasa ni magumu, ugumu ambao kama mtu atabweteka na kushindwa
kutimiza wajibu wake ipasavyo upo uwezekano mkubwa wa kujikuta anaingia
katika mfumo wa maisha yasiyokuwa na mbele wala nyuma na ugumu huo wa
maisha kuwa mara mbili yake.
Lakini licha ya ukweli huo, bado nafasi zipo wazi kwa watu kuingia
katika ulimwengu wa mafanikio. Hii itatokea tu kama mtu ataamua
kupambana ipasavyo na kuhakikisha haingii katika kapu la umaskini ambalo
limejaa wengi hata wasiostahili kuwemo ndani ya kapu hilo.
Wapo watu na afya zao, nguvu za kutosha pamoja na maarifa waliyopewa
na Mungu lakini bado wameridhika kuishi maisha ya kifukara huku
wakitegemea misaada kutoka kwa watu wengine ili kuweza kusogeza siku.
Hakika hii ni hatari sana na uhatari huo unakuja hasa pale unapomuona mtu ambaye ana kila
sababu ya kuwa miongoni mwa watu wenye mafanikio lakini yeye anaona
hawezi kuwa hivyo huku akiwa na dhana kwamba, yeye ni miongoni mwa wale
waliopangiwa kuishi maisha ya kifukara hadi mwisho wa maisha yao.
Wapo wanaoamini kwamba, Mungu kaleta ulimwenguni watu wa sampuli mbili. Yaani kuna maskini ambao hata wafanye nini hawawezi kuwa matajiri na kuna matajiri ambao wao wamepangiwa neema ‘mwanzo mwisho’.
Watu wanaofikiria hivyo wapo huko mtaani, yaani wao wanaamini kwamba
wameumbwa na umaskini na hawezi kufanya chochote kitachoweza
kuwabadilisha kuwa miongoni mwa matajiri.
Wenye dhana kama hizi ndiyo wale tunaowaona huko mtaani wakiishi
maisha wasiyostahili kuishi.Mtu kama ni kilema asiye na mikono wala
miguu, anaweza
kuwa sahihi akisema hana kitu anachoweza kukifanya akawa tajiri
kutokana na udhaifu aliokuwa nao lakini wewe ambaye umejaaliwa kuwa
miongoni mwa waliojaaliwa kuwa na viungo kamili, nguvu pamoja na maarifa
iweje ujione kwamba uko sawa kuishi maisha duni?
Huoni kwamba utakuwa unajidhalilidha? Jamani ifike wakati ukae chini
na ujiulize sababu za wewe kuendelea kuishi maisha mabaya wakati wenzako
kila siku wanapiga hatua mbele.
Huenda kuna sehemu unakosea hivyo ni vyema ukaibaini na kufanya
mabadiliko ya haraka ili na wewe uweze kuwa miongoni mwa wale waliotumia
vizuri nafasi zao za kuletwa hapa ulimwenguni.
Kama unataka kutimiza wajibu wako wa kuletwa hapa ulimwenguni una
kila sababu ya kufanya kazi kwa bidii bila kuridhika na hicho kidogo
unachokipata sasa. Siku zote ota kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa
duniani bila kujali kwa sasa uko katika nafasi gani.
Nasema hivyo kwasababu, kuna wanaodhani kwamba kwa kuwa sasa hivi ni
maskini watakuwa wamechelewa na uwezekano wa wao kuwa matajiri haupo
tena.
Lahasha!
Siku zote mbio za kuelekea kwenye utajiri huanzia
kwenye mstari wa umaskini kwa maana hiyo, hapo hapo ulipo anza kukimbia
kwa spidi kubwa huku ukiwa na malengo ya kuwa wa kwanza kuuvuka mstari
wa kuingia kwenye mafanikio.
Yaweza kuwa kama ndoto ya mchana vile kwa mtu fukara kuamini kwamba
akiamua ipo siku anaweza kuuaga umaskini lakini amini inawezekana.
Na hii inatokana na ukweli kwamba, matajiri wengi wakubwa ukijaribu
kufuatilia historia zao utakuta walitokea kwenye umaskini lakini
wakausaliti na sasa ni miongoni mwa watu wenye mafanikio makubwa.
Sasa wewe unasubiri nini? Ni wakati wako sasa wa kubadilika.
Kikubwa cha kuwa nacho ni hasira ya kufanikiwa. Yaani uwe na shauku kubwa ya kuwa kama hao wenye mafanikio makubwa.
Unapowaona, kuwasikia ama hata kusoma habari
zao kuwa na wivu, wivu ambao mwisho wa siku utakufanya nawe kuwa kama
wao. Said Bakhresa wa Tanzania na Bill Gates wa Marekani (pichani) ni
miongoni mwa watu wenye mafanikio makubwa duniani.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment