WANANCHI: UKAWA WARUDI BUNGENI ILA WASIPUUZWE.


Baadhi ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao wamesusa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Na MWANDISHI WETU
WANANCHI mbalimbali jijini Dar es Salaam wamelitaka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao wamesusa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma, kurejea bungeni ili kusaidia kupatikana kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalum, wananchi hao walisema wakati wanawasihi Ukawa kurejea, lakini wamewataka pia wajumbe wengine wanaoendelea na vikao hivyo, kuacha kuwabeza wapinzani hao waliodai baadhi ya hoja zao zina mashiko.
“Mimi siungi mkono kitendo cha Ukawa kutoka nje ya Bunge, lakini ninawaona wanazo hoja za msingi ambazo kama zingezingatiwa nchi yetu ingeweza kupata katiba nzuri. Ninawasihi warudi ila wenzao wa CCM nao wasiwabeze kwa kila jambo, wachukue vitu vizuri vibaya waviache, hii ni katiba ya Watanzania wote,” alisema Sabas Salibinius, mkazi wa Buguruni, jijini Dar es Salaam.
“Mimi nawaunga mkono Ukawa, lakini wakiwa ndani ya Bunge, sipendi watoke, wakae watoe hoja zao tuzisikie. Kitendo chao cha kutoka nje kwa kweli siyo kizuri. Lakini pia niwasihi wajumbe wa CCM, wasitumie uwingi wao vibaya, wenzao wakirudi wasiwabeze, wawasikilize hoja zao halafu nao wajibu kwa hoja,” alisema Kibiti Samiti mkazi wa Kimara Mwisho.
Aidha, watu wengine waliohojiwa kuhusu kususa kwa Ukawa bungeni, walisema siyo jambo jema kwa nchi, kwa vile kutasababisha kushindwa kupatikana kwa katiba mpya yenye masilahi kwa Watanzania wote, kwa sababu itakuwa imeandikwa kwa mawazo ya watu wa upande mmoja. 
Share on Google Plus

About ahmed

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment