BAHATI
mbaya sana, simjui huyu bwana mdogo, anayekwenda kwa jina la Nuhu
Mziwanda, aliyekuwa rafiki wa kiume wa msanii anayekimbiza katika muziki
wa mduara, Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole.
Naambiwa naye ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, ingawa sijawahi
kuisikia kazi yake yoyote. Lakini nikiri kuwa nimeiona picha yake mara
nyingi, akiwa na mpenziwe na hata na watu wengine. Ni kijana mtanashati
anayeweza kuwavutia wasichana wanaopenda mabrazamen!
Kwa muda mrefu, Nuhu na Shilole walikuwa wakiishi pamoja kama mtu na
mpenzi wake. Mara kadhaa, yamewahi kuibuka madai kuwa kijana huyo
alikuwa ni mdogo kiumri kwa msichana, lakini mara zote, mkali huyo wa
kibao cha Paka la Baa amekuwa akikataa.
Binafsi aliwahi kuniambia wanaosema umri mdogo wa mpenzi wake, ni
wambeya, wanamuonea wivu, kwa sababu yeye ana umri sawa na mwenzake.
Haina ubishi kwamba walipendana na ili kuwathibitishia watu hivyo, Nuhu
alijichora tatoo kwenye paja la mkono wake, akiwa ameandika maandishi
yanayosomeka Shishi Baby, jina lingine la kisanii la Shilole!
Lakini katika hali isiyotarajiwa, penzi la Shilole na Nuhu
likaparanganyika ghafla. Ni hapa ndipo ninapotaka kujikita leo
ninapozungumza na huyu bwana mdogo. Najua, umri wake bado mdogo, hivyo
kuna mambo mengi kwake ni mageni na asiyo na uzoefu nayo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tatoo aliyojichora Nuhu, ni ile ambayo
haiwezi kufutika, kwa maana hiyo pamoja na kupigwa kibuti, Shishi Baby
itaendelea kung’ara mkononi mwake na kila siku ataiona.
Moja kati ya
vitu ambavyo mtu anapaswa kuviogopa na kuwa na tahadhari kubwa kabisa
ni mapenzi, hasa haya ya kizazi cha sasa chenye kupenda kuiga, anasa,
utanashati na kulelewa (Shugamami na shugadadi).
Mapenzi yamesababisha wengi kuharibu maisha yao na kama mnavyojua,
watu wanauana kila siku, mke au mume anamuua mwenzake, tena wakati
mwingine, kikatili kabisa. Mapenzi ya siku hizi yanahitaji ‘timing’.
Uaminifu, siyo tu ule wa kutotoka nje ya ndoa, bali kupendana kwa dhati
ya moyo, haupo.
Watu wanapendana kulingana na upepo unavyokwenda, leo wanashibana sana, kesho chui na paka.
Hatukatai kuonyeshana mapenzi, tunawaona watu ufukweni kila siku
wameshikana viuno, wanakulana denda hadharani na wakati mwingine hata
zaidi ya hapo. Ni wakati wao, unaruhusu kwa sababu ni nyakati za furaha.
Kesho wakigombana, kukumbatiana kwao jana ufukweni hakuonekani.
Kwanza, utamaduni wa kujichora tatoo binafsi huwa siupendi kwa vile
naamini siyo wetu, ni wa kuiga. Lakini kama ni kuongeza mapambo mwilini
kwa kuwa wao ni wasanii, zipo tatoo za kujichora kwa rangi, badala ya
hizi za kutoboa mwili. Siku ikikuchosha, unaitoa.
Halafu, nadhani kama ni kujichora kuonyesha mapenzi kwa mtu, watu
pekee wenye hadhi hiyo ni watoto wako, mama au baba yako. Hawa, vyovyote
itakavyokuwa, hata mgombane vipi, bado watabaki kuwa ni damu yako.
Nasisitiza tena, kila mtu ana haki ya kupenda atakavyo, lakini jambo
moja muhimu ambalo nina uzoefu nalo, mapenzi ya enzi hizi za dotcom ni
ya upepo. Kuna machungu mengi ambayo yanawafanya watu kujutia uamuzi wao
wa kuoa au kuolewa na walionao sasa. Wakati mababu zetu walizeekea
kwenye ndoa, asilimia chache sana ya vijana wa sasa wanaoweza, angalau
kukaa miaka kumi katika ndoa.
Sidhani kama kweli Nuhu alimpenda kihivyo Shilole na kama ndivyo,
nimpe pole na kumtahadharisha asije chora tena tatoo nyingine ya
mwanamke mwilini mwake, wanaume wenzake watamcheka!
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment