NUKUU ya kusikitisha aliyoiacha mwanafunzi Ezra Gerald
Wabamba aliyejinyonga katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera ilisomeka
hivi: “Haiwezekani binadamu kuhudumiwa kama mbwa, yaani nafika
hospitali naeleza hali yangu halafu daktari ananiandikia kulazwa bila ya
kupimwa, sasa sijui watatibu nini?
“Kwa kweli siwezi kuvumilia yaani wenzangu wanasoma halafu mimi
nimekalishwa tu hapa hospitalini bila ya kujua wananitibu nini, inaniuma
sana mpaka kufika hatua hii ya kujiondoa duniani, ni kwa sababu
ninaona wanachezea ndoto zangu, mimi siwezi kuona ndoto yangu inazimwa
wakati ninatakiwa niwepo shuleni nikamilishe ndoto zangu, mjitahidi
tukutane mbinguni.”
Kwa mtu mwenye kujali ujumbe huu ni mzito sana, hauwezi kupuuzwa kwa namna yoyote kwa sababu una msingi wa malalamiko ya kila
siku juu ya matibabu katika hospitali zetu nchini. Kwa wanaoacha upepo
wake upite wanaweza wasione madhara, lakini dunia imeshuhudia hivi
karibuni serikali ya Tunisia ikiangushwa madarakani kwa sababu ya muuza
matunda.
Mchuuzi huyo wa matunda aitwaye Mohammed Boaziz hakuonekana kuwa
tishio katika utawala wa Rais Ben- Ali wa nchi hiyo, kama ambavyo kifo
cha Ezra kinavyoweza kuchukuliwa.
Tafsiri inayowafanya wakuu wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni: “Mtoto mwenyewe ni mwanafunzi tena
anatoka katika familia maskini ambayo haiwezi kufanya chochote cha
kudhuru nafasi zetu za uongozi.”
Kasumba hii ndiyo aliyokuwa nayo Ben Ali
na wasaidizi wake, aliwachukulia watu maskini kama vikaragosi ambao
hawawezi kuwa na madhara katika utawala wake, dola iliwaonea itakavyo,
machozi ya walalahoi yalichukuliwa sawa na ya samaki kuishia baharini
lakini kauli ya Ezra ya ‘tukutane mbinguni’ ina maana kubwa sana.
Wengi huamini mbinguni ndiko kuliko na haki, imani ambayo Boaziz
wakati akijilipua kwa petro aliamini pia kuwa bora atangulie kwa mtoa
haki ili waliomtesa watakapokwenda huko wahukumiwe kwa dhuluma zao.
Lakini wakati imani hiyo inaheshimiwa hasa na wenye dini, kuna baadhi
husema malipo ya haki hulipwa hapahapa duniani, naamini hivyo kwa
ushahidi uliotokea Tunisia.Kinachoniogopesha ni mkondo huo kuikumba nchi
yangu pia. Maana yaliyokuwa yakifanywa na watawala wa nchi hiyo
yameanza kufanyika hapa, haki ya raia haipatikani kirahisi. Malalamiko
yaliyomuondoa Ezra duniani siyo mageni, serikali inajua kuwa hospitali
zake nyingi huduma zimezorota kwa kiwango kikubwa. Wagonjwa wanalazwa
bila kupewa huduma stahili.
Nilidhani tukio la kifo cha Ezra lingechukuliwa kama mwanzo wa safari
ya wizara kujisafisha, lakini wasemaji wake waliniambia kuwa tukio hilo
hawawezi kulizungumzia kwa sasa kwa sababu limeshakuwa jinai.
Hilo halizungumziki kwa sababu hiyo, je malalamiko mengine ambayo
yanatolewana na wagonjwa juu ya kukosekana kwa dawa hata za kutuliza
maumivu kwenye hospitali nyingi za serikali ikiwemo ya Palestina,
Mwananyamala zilizopo jijini Dar es Salaam na karibu hospitali nyingi za
mikoa hali ya matibabu haziridhishi hata kidogo, vipi hiyo nayo ni
jinai isiyozungumzika?
Ushauri wangu kwa serikali, pamoja na kukipuuza kifo cha mwanafunzi
huyo kama ukimya unavyoendelea hivi sasa, desturi hii ya kutokujali
vilio vya wanachi iachwe kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda wafuasi wa
kupigania haki zao wanaongezeka. Leo mtawazima kwa mabomu na risasi za
moto lakini Tunisia walishindwa kuwatuliza kwa ndege za kivita na
vifaru.
Mwisho Wizara ya Afya ifuatilie kwa ukaribu tukio la kifo cha Ezra na
kutoa ripoti ambayo itawaacha huru wananchi kutoka kwenye hisia za
vilio vyao kupuuzwa na kuamini kuwa serikali yao inawajali. Nachochea
tu!
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment