Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy wiki iliyopita alilazimika
kusindikizwa na askari wa Bunge la Jamhuri kuondoka katika viwanja vya
eneo hilo kumnusuru na hasira za wajumbe kutoka Zanzibar waliokerwa na
mchango wake kuhusu masuala ya Muungano.
Kessy alisimama bungeni hapo kutoa mchango wake kuhusu Katiba ya Jamhuri akijikita zaidi katika suala la muundo wa Muungano na kusema kwamba Zanzibar inabebwa na Tanganyika.
Nimnukuu, alisema: “Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanganyika inabeba mzigo
mkubwa ambao haubebeki, hapa tunahudumia wabunge 83 kutoka Zanzibar
ambao wanatibiwa wao na wake zao na watoto kwa gharama za Tanganyika
wakati hawachangii.”
Aliongeza kuwa haiwezekani kwa Tanganyika kubeba mzigo mkubwa kama huo wakati katika Jimbo lake
la Nkasi wananchi wanalia na shida ya maji.Alisema katika kamati yao
Namba Moja, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu alitoa semina
iliyoonyesha kuwa Zanzibar haichangii chochote kwenye Serikali ya
Muungano na kuwa hata mishahara wakati mwingine wanategemea Tanganyika.
Kessy alisema wananchi wakilijua jambo hilo, wataikataa katiba
inayopendekezwa na kuitupilia mbali kwa kuwa inatoa upendeleo kwa
Wazanzibari na kuikandamiza Tanganyika.
“Mimi naweza kuwa na wanawake sita, nikazaa nao lakini kila
mtoto anaendelea kutunzwa na baba yangu, jambo kama hili halivumiliki
hata kidogo japo najua kuwa ukweli unawauma,” alisema huku baadhi ya
wajumbe wakipaza sauti wengine kumpinga na wengine kuomba mwongozo wa
mwenyekiti.
Lakini ninachotaka kusema hapa ni kwamba wananchi wengi wa Tanganyika
niliozungumza nao katika utafiti wangu usio rasmi wanaungana na mbunge
huyo.
Hapa Dar es Salaam baadhi ya wakazi wanasema iweje Zanzibar yenye
watu milioni moja na ushee wawe na wabunge 83 wakati jiji lao lina
wakazi zaidi ya milioni nne na lina wabunge wasiozidi kumi?
Alipinga
suala la Rais wa Zanzibar kuwa makamu wa rais wa Muungano kwa maelezo
kuwa katika mfumo wa vyama vingi jambo kama hilo haliwezekani na kuhoji
itakuwaje awe makamu wa kwanza wa rais wakati hajachaguliwa na wananchi
wa Tanzania Bara?
Baada ya kauli hiyo, kelele za wajumbe kutoka Zanzibar ziliongezeka
baadhi wakisimama na kuwasha vipaza sauti kumshambulia Kessy hivi:
“Chizi huyo, chizi huyo, hafai kwanza ni Mwarabu,” zilisikika sauti huku
nyingine zikimtaka aombe radhi.
Ukweli ni kwamba alichokizungumza Kessy ndizo kero za muungano kwa
upande wa Tanganyika. Kati ya watu 50 niliowauliza jijini Dar kuhusiana
na kauli hizo, ni wawili tu waliopingana naye, hivyo ni dhahiri kwamba
kauli yake inapaswa kutazamwa.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba wachache wakitokea na kutoa wazo ambalo baadaye linaweza kuleta vurugu, ni bora likakubaliwa kama halina madhara. Hivyo hayo ya Kessy yatazamwe na yasipelekwe kisiasa.
Sikuona sababu za wajumbe kutoka Zanzibar kumshambulia Kessy wakati
aliyesema hayo ni Gavana wa Benki Kuu, Bwana Ndulu yeye alikuwa akirudia
na ndiyo maana akasema hayupo tayari kuomba radhi.
Alidai Ndulu
alikuja katika kamati na akasema kwamba tangu kifo cha Abeid Karume
(rais wa kwanza wa Zanzibar), Zanzibar hawajawahi kuchangia muungano,
hili lilikuwa ndilo la msingi la kulijadili kama ni kweli au ni uzushi
na siyo kuzomea na kutaka kumpiga mtoa hoja.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment