Membe: Bila kufuli la CCM pasingetosha urais 2015

    Uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM wa kuwadhibiti kwa mwaka mmoja makada wake sita waliobainika kukiuka kanuni kwa kuanza mapema kampeni za urais, unaweza kuwa uliwakera wengi, lakini si Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ambaye ni mmoja wa ‘waliofungwa kufuli’.
Membe anaona adhabu hiyo ilikuwa mwafaka na kwamba laiti uamuzi huo usingefanywa mapema, “ingekuwa vurugu tupu”.
“Sijui nchi hii ingekuwa wapi kama watu wangeachwa bila ya kuwekewa ‘gavana’,” alisema Waziri Membe kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika kwenye ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Membe pamoja na makada wengine, Frederick Sumaye, Edward Lowassa, William Ngeleja, Stephen Wasira na January Makamba walibainika kukiuka kanuni za uongozi na maadili za CCM kwa kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Kwa mujibu wa taarifa ya CCM iliyotolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu, makada hao walikiuka kanuni za uongozi na maadili za CCM kwa mujibu wa Toleo la Februari 2010 Ibara 6 (7) kwa baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Bila ya kueleza ni jinsi gani vurugu hizo zingefanyika, Membe alisisitiza kuwa vurugu ingekuwa kubwa kama chama hicho kisingechukua hatua mapema.
“We angalia, kuna makundi mawili. Hili kundi letu (la walioanza kampeni mapema wakaadhibiwa) na hili jipya la hawa ambao wameanza kujitokeza sasa, ingawa najua nao watadhibitiwa tu. Hawa wasingedhibitiwa, ingekuwaje?” alihoji Membe.
Wakati CCM inawaita makada hao kwa ajili ya kuwahoji, tayari baadhi walishaanza kufanya sherehe na kualika wenyeviti wa mikoa ambao walieleza misimamo yao juu ya mgombea urais wanayemuunga mkono, wengine kuzunguka kwenye hafla mbalimbali kwa ajili ya harambee na wengine kuzigawa jumuiya za chama hicho, hasa Umoja wa Vijana (UVCCM), huku baadhi ya vikao vikiripotiwa kutawaliwa na malumbano yaliyosababishwa na misimamo tofauti kuhusu mgombea urais wa CCM.
Hata hivyo, Waziri Membe (61) hakusita kukosoa muundo wa vyombo vya uamuzi vya CCM ambao unawapa fursa baadhi kushiriki katika kuadhibu wanaotaka nafasi fulani na baadaye walioadhibu kujitokeza kuwania nafasi hiyo akisema utaratibu huo unawaonea wale ambao hawana fursa ya kuwadhibiti wengine.
“Chama chetu sasa kiwe na utaratibu unaowabana watu fulani kugombea kutokana na nyadhifa zao. Kwa mfano, uko kwenye nafasi ya kufanya uamuzi, unawaadhibu hawa halafu baadaye unajitokeza wewe. Huwezi kuchuja halafu ukajitokeza wewe (kugombea). Kutakuwa hakuna objectivity (haki),” alisema bila ya kuweka bayana watu waliohusika katika kuadhibu na baadaye wakajitokeza kuwania urais.
“Tuwe na utaratibu kwenye chama kwamba wanaowabana watu fulani, wasigombee na hasa wale walioshiriki uamuzi ule na wengine walioko kwenye nafasi za uamuzi… Kamati Kuu na hata (Halmashauri Kuu) Nec na Kamati ya Maadili, nao wasije kujitokeza baadaye na kutangaza nia. Vinginevyo hatutawaelewa,” alisema.
Pamoja na kusifu kitendo cha Kamati Kuu kudhibiti makada mapema, Membe anaona muda umefika kwa CCM kuruhusu wanachama wake wanaowania urais waanze harakati zao sasa.
Share on Google Plus

About ahmed

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment