SIMBA jana Ijumaa iliondoka kwenda Unguja, Zanzibar kuweka kambi
yake kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Bara huku ikimwacha
mshambuliaji wake Mkenya, Paul Kiongera aliyepo Nairobi na anatarajia
kujiunga na timu hiyo wiki ijayo. Yanga nayo itatua Zanzibar Jumatatu.
Simba ilimalizana na Kiongera lakini ilimruhusu
kurudi kwao kuisadia timu yake ya KCB katika mechi za Ligi Kuu Kenya
(KPL) ili iepukane na hatari ya kushuka daraja kutokana na kupata
matokeo mabaya kwenye mechi zake za awali.
Kwa sasa Simba ipo chini ya kocha mpya Mzambia
Patrick Phiri ambaye alianza kazi ya kuifundisha mara baada ya kusaini
mkataba wa mwaka mmoja juzi Alhamisi. Simba iliondoka jana saa 10 jioni
kwa boti ya Azam Sea Express.
Akizungumza na Mwanaspoti, Rais wa Simba, Evans
Aveva, alisema timu itakaa huko mpaka ligi itakapoanza ingawa alidai
kuwa endapo kutakuwapo na mechi za kirafiki watakuja jijini kucheza na
kurudi Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment