MADRID, HISPANIA
KILA
sehemu kuna wazee wenye busara, hata kama sio wazee kiumri. Mchambuzi
maarufu wa soka la Hispania anaamini kuwa huu ndiyo utakuwa msimu wa
mwisho kwa Cristiano Ronaldo kukipiga Santiago Bernabeu.
Guillem
Balague, mchambuzi maarufu wa soka la Hispania anaamini kuwa huu ni
msimu wa mwisho kwa Ronaldo Santiago Bernabeu na ingawa mwenyewe mapema
wiki hii alidai kwamba anataka kucheza Real Madrid mpaka mwisho wa
maisha yake ya soka, lakini Balague anaamini kuwa Ronaldo anaenda
Ufaransa kuichezea PSG.
Balague
anaamini kuwa wawakilishi wa Real Madrid na wawakilishi wa Ronaldo wote
wana furaha kuona staa huyo inabidi asonge mbele na maisha mapya baada
ya kufanya mambo mengi makubwa akiwa Santiago Bernabeu.
“Anaweza
kucheza mpaka akifikisha miaka 40, lakini kuna mkakati maalumu kutoka
kwa watu wake. Inaonekana huu utakuwa msimu wa mwisho kwa Cristiano
Ronaldo Real Madrid. Inaonekana pia kuwa Madrid siyo kwamba hawana
furaha na suala hilo,” alisema Balague.
Juzi
Ronaldo alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-0 wa Real Madrid
dhidi ya Levante katika Ligi Kuu ya Hispania La Liga na kwa kufanya
hivyo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia
ya Real Madrid.
Hilo
lilikuwa bao la 324 katika mechi 310 alizoichezea Real Madrid akivunja
rekodi ya mkongwe wa timu hiyo, Raul Gonzalez aliyefunga mabao 323
katika mechi 741 alizoichezea miamba hiyo ya Santiago Bernabeu. Msimu
uliopita, Ronaldo ambaye ni hasimu mkuu wa staa wa Barcelona na timu ya
taifa ya Argentina, Lionel Messi aliifungia Real Madrid mabao 48 katika
mechi 35 na kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa mabao barani Ulaya.
Balague
anaamini kuwa staa huyo wa kimataifa wa Ureno ambaye Februari 5 mwakani
atatimiza miaka 31 ataelekea nchini Ufaransa katika hatua nyingine
muhimu ya maisha yake ya soka.
“Inaonekana
ni kitu cha kushangaza sana unapoangalia rekodi ambazo amezipata,
ikiwemo kuwa mmoja kati ya wafungaji bora zaidi duniani. Lakini labda
Real Madrid inaamini kuwa ameshafika kileleni na nina hisia kwamba PSG
ndiyo itakuwa chaguo lake kubwa. Naamini ni katika kipindi kijacho cha
majira ya joto. Sidhani kama atakuwa Real Madrid kwa muda mrefu,”
aliongeza Balague.
Ronaldo
alinunuliwa na Real Madrid kwa dau la Pauni 80 milioni kutoka
Manchester United Juni 26, 2009 huku akivunja rekodi ya uhamisho na kuwa
mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka duniani huku akisaini
mkataba wa miaka sita.
Mkataba
wake kwa jumla ulikuwa na thamani ya Euro 11 milioni kwa mwaka na
kulikuwa na kipengele ambacho kingemruhusu kuondoka klabuni hapo kama
kuna timu ingefikia dau la Euro 1 bilioni. Alikabidhiwa jezi namba 9 na
mkongwe wa Real Madrid, Alfredo Di Stefano huku akitambulishwa Santiago
Bernabeu mbele ya mashabiki 85,000 na kuvunja rekodi iliyowekwa na staa
wa zamani wa Argentina, Diego Maradona ambaye alitambulishwa mbele ya
mashabiki 75,000 wakati alipohamia Napoli kutokea Barcelona mwaka 1984.
0 comments:
Post a Comment